Social Icons

mfuko wa pensheni wa pspf

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Featured Posts

Monday, November 24, 2014

KAMPUNI YA MABATI YA ALAF YATOA MSAADA WA MABATI KWA AJILI YA UJENZI WA MAABARA ZA SHULE ZA SEKONDARI WILAYA YA MBEYA.

 Meneja wa Kampuni ya ALAF Tawi la Mbeya, Greyson Mwakasege akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kabla ya kumkabidhi msaada wa mabati 384 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara.
 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King, akitoa shukrani kwa kampuni ya ALAF  kwa kujitolea mabati kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari za Wilaya ya Mbeya.
  Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King na Meneja wa ALAF tawi la Mbeya, Greyson Mwakasege wakikabidhiana mabati 284 kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za Kata.
 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King akiwaonesha waandishi wa habari(hawapo pichani) msaada wa mabati aliyokabidhiwa na Kampuni ya ALAF .
 Meneja wa ALAF tawi la Mbeya, Greyson Mwakasege akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya bidhaa zingine zinazozalishwa katika kiwanda cha Mbeya.

 Fundi umeme na mtaalamu wa Mashine wa Kiwanda cha kuzalisha mabati, Himid Mwenzegule akiendelea kuendesha mitambo ya mashine ya kuzalisha mabati kiwandani hapo.
 Mashine ya kuzalisha mabati ya migongo ya kawaida aina ya Corrugator ikiendelea na kazi.
 Mashine ya kuzalisha mabati ya migongo mikubwa aina ya IT.
 Mashine ya kuzalisha vigae aina ya Versa Tile
 Mabati aina ya Simba Dumu yaliyozalishwa kiwandani hapo.
 Baadhi ya mabati yaliyozalishwa kiwandani hapo yakiingizwa kwenye Roli tayari kuelekea sokoni kwa wateja.


KAMPUNI ya mabati ya ALAF imetoa  msaada wa mabati 384 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za shule za Sekondari za Wilaya ya Mbeya zenye thamani ya shilingi Milioni 7.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King,Meneja wa Tawi la Mbeya Greyson Mwakasege, alisema walipokea maombi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara katika Shule za Kata.
Alisema walikubaliana na ombi hilo na kuona ni vema kusaidia Bandle 32 sawa na mabati 384 yenye thamani ya Shilingi Milioni 7 baada ya mabati hayo kuanza kuzalishwa katika Kiwanda cha Mbeya ambacho pia kinahudumia Mikoa ya Ruvuma, Katavi, Rukwa,Njombe, Iringa na Mbeya.
Alisema ni matarajio yao ya kuendelea kusaidia maeneo mengine kama mchango wa Kampuni kwa jamii inayowazunguka pamoja na kuthamini wateja wake ambao hupata huduma kutoka katika kiwanda cha Mbeya.
Mwakasege aliongeza kuwa katika Kiwanda cha Mbeya kina mashine tatu ambazo ni Mashine aina ya IT inayotengeneza mabati ya migongo mikubwa, Mashine aina ya Corrugator inayozalisha mabati yenye migongo ya kawaida midogo pamoja na mashine aina ya Versa Tile inayozalisha vigae aina ya Versa.
Alizitaja bidhaa zingine zinazopatikana kuwa ni pamoja na Bati za Afrika kusini na vigae vyenye rangi za Bluu, Kijani na Nyekundu,Nondo kutoka Uturuki, Black Pipe, Z parlin na Hollow section.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King, mbali na kutoa shukrani kwa Kampuni ya ALAF  kwa msaada wa mabati pia alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Mbeya kujenga utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo ya Wilaya.
Alisema mabati hayo yatasaidia katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Galijembe ambayo imeteuliwa na Wilaya kuwa Shule ya Bweni ya wasichana kutokana na ujenzi wa maabara kukamilika kwa asilimia kubwa.
Alisema lengo la kuiteua shule ya Galijembe kuwa shule ya Wasichana ya bweni ya Wilaya ni kuwaondolea adha watoto wa kike ambao asilimia kubwa wanaumri mdogo kwenda uaraiani kupanga vyumba baada ya kufaulu kujiunga na sekondari.
Alisema wasichana wanapata madhara makubwa wakiwa wamepanga kwenye nyumba uaraiani yakiwemo Mimba za utotoni na magonjwa ikiwa ni pamoja na kupunguza hali ya ufaulu darasani kutokana na mazingira hivyo Wilaya ya Mbeya imejipanga kuhakikisha hilo linaondoka.


KITUO CHA MSAADA WA KISHERIA(MBEPAU) CHA TOA MAFUNZO KWA WASAIDIZI WA KISHERIA 25 MBEYA.

 Mkufunzi,Nuhu Suleiman kutoka Chuo kikuu cha Mzumbe akiwafundisha vijana mafunzo ya msaada wa kisheria kwa Wasaidizi wa kisheria 25 kutoka Jiji la Mbeya.         Vijana Wakipata mafunzo
KATIKA kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, vijana 25 wamepatiwa mafunzo ya wasaidizi wa kisheria Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Msaada wa kisheria cha Mbeya Paralegal Unit(Mbepau), Jane Lawa, aliliambia gazeti hili kuwa kituo chake kimeona kutoa mafunzo kama hayo kutokana na kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto na wanawake mkoani Mbeya.
Alisema mafunzo hayo yametolewa kwa vijana 25 kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya yaliyoanza Novemba 17 na kufungwa Novemba 21, Mwaka huu katika ukumbi wa Coffee Garden uliopo mjini hapa kwa ufadhili wa Legal Services Facility(LSF) mafunzo yaliyofundishwa na Mtaalamu kutoka Chuo kikuu Mzumbe.
Lawa alisema lengo la kutoa mafunzo kama hayo kwa vijana ni kupanua wigo wa kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria kutoka ngazi ya kaya kwa kuwa vitendo vingi huwakumba watu maskini lakini wanashindwa kutoa taarifa kutokana na kutoelewa njia sahihi ya kupita na kupata msaada.
Aliongeza kuwa Jiji la Mbeya pekee  linaKata 36 lakini vijana waliojitokeza ni kutoka Kata 25 tu jambo linalosababishwa na vijana kukataa kufanya kazi za kujitolea na kutanguliza maslahi mbele hivyo kupelekea idadi ndogo ya vijana kujitokeza katika mafunzo hayo.
Baadhi ya vijana waliopatiwa Mafunzo hayo walisema wamepata manufaa kutokana na kuongeza uelewa juu ya masuala ya kisheria na kuahidi kusaidiana na asasi zingine kupiga vita ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa kutoa elimu na misaada ya kisheria pindi itakapohitajika.
Mathias Halawa kutoka kata ya Mabatini na Halima Mbelwa kutoka Kata ya Forest walisema kupitia mafunzo hayo wataweza kuwasaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa kuwashauri njia za kupita ili waweze kupata haki zao kwa muda unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kwenye vyombo vya Sheria kama Polisi na Mahakamani.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo, Nuhu Suleiman kutoka Chuo kikuu Mzumbe Tawi la Mbeya, alisema ili kuboresha na kupanua  huduma za msaada wa kisheria ni vizuri kujenga ushirikiano na taasisi zote zinazofanya kazi za namna hiyo kama Jeshi la Polisi na Mahakama pamoja na Wanasheia wa Serikali na Mawakili.
Alisema vijana hao amewafundisha Haki za binadamu, Ulinzi wa haki za binadamu hususani za Wanawake kama kundi maalumu, ukatili wa kijinsia na ujengwaji wa uwezo kisheria ili waeze kuongeza upana wa uelewa wa masuala ya kisheria kwa jamii wanazotoka.
Na Mbeya yetu

UNAJUA CHIMBUKO LA AKAUNTI YA ESCROW NA NANI ANACHEZESHA NGOMA YA ESCROW NA IPTL? SOMA HAPA KUJUA UNDANI WAKE


Kwa muda sasa kumekuwapo na tuhuma zinazohusu "wizi" wa fedha za akaunti ya escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2006. Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Chimbuko la akaunti hiyo ni mgogoro wa tozo hiyo kwamba iligubikwa na utata baada ya kudaiwa kwamba Tanesco ilikuwa ikitozwa fedha nyingi kuliko inavyostahili.
           
Tuhuma za huo "wizi" hata hivyo hazikuishia tu kwa wahusika wakuu yaani makampuni ya umeme, bali zimetiririshwa hadi kwa watu binafsi ambao kimsingi hawana uhusiano wowote na mgogoro huo wa malipo na wala kuhusika kwa njia yoyote na hicho kinachodaiwa kwamba ni uporaji wa fedha za akaunti hiyo ya Escrow. 

Akaunti Escrow ni akaunti ya amana ambayo inawekwa chini ya uangalizi wa mtu wa tatu ili huyo mwangalizi aikabidhi kwa mlengwa pale tu masharti kadhaa yatakapokuwa yamekamilishwa. Hivyo basi akaunti hiyo maalum ya amana ilifunguliwa na kuwekwa chini ya Benki Kuu kama wakala anayesubiria kutekelezwa kwa masharti maalumu ili aikabidhi kwa wenye kumiliki fedha hizo watakapomaliza tofauti zao.


   
Ni vizuri kuliangalia suala hili la akaunti maalum ya amana kwa namna ambayo itawafanya wale wenye kiu ya kutaka kujua ukweli kukidhi hamu yao. 

Fedha iliyokuwa ikiwekwa katika akaunti hiyo ni tozo ya uwezo wa mitambo ya kufua umeme ambayo kampuni ya IPTL ilikuwa ikiitoza Tanesco. Baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kupunguza tozo ya IPTL kutoka USD 3.6million kila mwezi mpaka USD 2.6million kila mwezi baadaye TANESCO ilishauriwa vibaya na wanasheria kwamba tozo hiyo bado ni kubwa kuliko mkataba baina ya IPTL na TANESCO Mei 26, 1995 unavyo eleza.
          
Ubishani uliozuka kati ya mtoa huduma ya umeme yaani IPTL na mtumia huduma ya umeme yaani Tanesco ndio uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo maalum ya amana yaani escrow account katika Benki Kuu ya Tanzania {BoT} kama njia salama ya kutunza fedha hizo hadi mgogoro utakapokuwa umetatuliwa. 

Ni muhimu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba mtoa huduma yaani IPTL hasitishi kufua umeme na mtumiaji wa umeme yaani Tanesco naye hakosi umeme wa kuuza kwa walaji wake. Hiyo ni busara ya kibiashara. Fedha hizo zililipwa katika akaunti hiyo maalum kutokana na hati za madai au ankara kutoka kwa mtoa huduma na si vinginevyo.
          

Sunday, November 23, 2014

WATU ZAIDI YA 25 WAJERUHIWA VIBAYA KATIKA AJALI YA COSTA SENJELE MBEYA.Baadhi ya majeruhi wakitafuta mizigo yao mara baada ya kutoka ndani ya basi hilo


Baadhi ya majeruhi wakitoka ndani ya basi hiloBaadhi ya abilia wakitaka kumpiga Dereva wagari ya aina ya Suzuki kuwa yeye ndio alisababisha ajali hiyo kwa kuyumbayumba kwake barabarani

Moja ya wasamaria wema akiwazuia abiria wenye hasira kali kutaka kumpiga mzee huyo Mwenye Suzuki ambae alijulikana kwa jina moja tu mzee Mtawa

Mwandishi wa habari Kenneth Mwazembeakiwasili katika Hospitali ya Ifisi akisindikizwa na  Joseph Mwaisango  wa Mbeya yetu baada ya kupata ajali eneo la Senjele wilayani Mbozi  akiwa anatokea shambani kwake  huko wilayani  Momba kwa taarifa za awali inasemekana amevunjika mguu wa kushoto
WATU zaidi ya 25 wajeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea jana baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Costa kutoka Mbozi kuelekea Mbeya kupinduka katika eneo la  Senjele wilayani Mbozi Mkoa wa Mbeya.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Costa lenye namba za usajili T 336 CJY ambalo lilipinduka baada ya kumshinda dereva wakati akijaribu kulikwepa gari linguine aina ya Suzuki lenye namba za usajili T 327 ARZ.

Kwa mujibu wa baadhi ya majeruhi walionusurika kwenye ajali hiyo walisema chanzo ni dereva kushindwa kulimudu gari la abiria baada ya kulikwepa gari dogo kutokana na kuwa na mwendokasi pamoja na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha.

Baadhi ya majeruhi walikimbizwa katika Hospitali teule ya Ifisi na wengine wakipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwisho.

Picha na Mbeya yetuWednesday, November 19, 2014

BENKI YA NMB MBEYA YATEMBELEA KITUO CHA YATIMA CHA MALEZI YA HURUMA NA KUTOA MISAADA MBALI MBALI.

Maafisa wa Benki ya NMB Mbeya wakishusha vitu kutoka kwenye gari kwa ajili ya kukabidhi msaada katika kituo cha watoto yatima Malezi ya Huruma Simike.

Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Mbalizi Road, Mzee Mwakibete, akikabidhi msaada kwa wanafunzi wa kituo cha watoto yatima cha Malezi ya Huruma Simike Mbeya.


Afisa biashara wa NMB Tawi la Mbalizi Road, Alex Massawe, akikabidhi msaada kwa wanafunzi wa kituo cha watoto yatima cha Malezi ya Huruma Simike Mbeya.

Mmoja kati ya Watumishi wa NMB tawi la Mbalizi Road akikabidhi msaada kwa wanafunzi wa kituo cha watoto yatima cha Malezi ya Huruma Simike Mbeya.


 Watumishi wa Benki ya NMB wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhi msaada.


Mmiliki wa kituo cha Malezi ya Huruma, Anah Kasire akitoa shukrani kwa niaba ya watoto.

WAFANYAKAZI wa Benki  ya Nmb tawi la Mbalizi road Mbeya wametembelea kituo cha watoto  yatima cha Malezi ya Huruma kilichopo Simike jijini Mbeya na kutoa misaada mbali mbali yenye thamani ya shilingi Milioni 1.1.

Afisa biashara wa NMB Tawi la Mbalizi Road, Alex Masawe alisema msaada waliotuo ni kutokana na wafanyakazi wa Benki hiyo kuguswa na maombi ya mmiliki wa Kituo hicho akiomba msaada wa vifaa vya shule kwa watoto wawili wanaoenda vyuo vya ualimu.

Alivitaja vitu vilivyopelekwa kuwa ni pamoja na Matranka mawili, makufuri mawili, Mchele debe tatu, mashuka 4, sabuni katoni 4, mafuta ya kula lita 20,sabuni ya unga kilo 20,nguo za ndani dazani 2, free style moja, mafuta ya kupaka dazani 2,miswaki dazani 5 na dawa za mswaki dazani 4.

Vingine ni vitambaa kwa ajili ya sare za chuo vya rangi nyeusi mita 6, mashati mawili, sabuni za kuogea dazani mbili, makaratasi aina ya manira 10, blanketi 4,unga wa sembe kilo 20, mahindi debe tatu, nyanya sado moja na vitunguu sado moja.

Masawe alisema hivyo vitu baadhi yake vitasaidia kituo na vingine ni kwa ajili ya wanafunzi waokwenda kusoma ambao sambamba na vitu hivyo pia walikabidhiwa fedha taslimu shilingi Laki moja na kufanya jumla ya vitu vilivyotolewa kuwa na thamani ya shilingi milioni 1.1.

bidii
Kwa upande wake Mmiliki wa Kituo hicho, Annah 
Kasire mbali na kuipongeza benki ya NMB kwa msaada huo alisema vitu hivyo vitaleta chachu kwa wanafunzi kuongeza katika masomo yao.

Aliwataja wanafunzi wanoenda kusoma kuwa ni Magreth Mwasile na Tumain Mwampamba ambao wote kwa pamoja wanatarajia kwenda kusoma Chuo cha Ualimu kilichopo Nyororo mkoani Iringa na kuongeza kuwa hadi sasa kituo kinalea watoto 120.

Mwisho.
Na Mbeya yetu

Tuesday, November 18, 2014

WAKULIMA WA MAZAO YA HORTICULTURE WAHAMASISHWA KUUNGANA.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Alfred Mzurikwao, akizungumza na wakulima mbali mbali alipokuwa amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbarali katika sherehe za Wakulima zilizofanyika katika skimu ya umwagiliaji ya Ilaji iliyoko Mbarali mkoani Mbeya.


Afisa wa TAHA, Isac Ndemanhile, akizungumza na wakulima zaidi ya 300 waliohudhuria sherehe za wakulima katika skimu ya Ilaji.

 Maafisa wa TAHA wakitoa maelezo kwa mgeni rasmi katika moja ya mashamba ya wakulima yanayoendeshwa kwa kufuata teknolojia mbali mbali.

Mkulima wa Nyanya, Daniel Wabare akionesha matunda ya shamba lake baada ya kupata elimu kutoka kwa maafisa wa TAHA.


 Baadhi ya wakulima wakiangalia mazao ya nyanya katika shamba la mmoja wa wakulima waliofundishwa na TAHA.

Baadhi ya wakulima kutoka skimu mbali mbali wakiwasikiliza maafisa wa TAHA wakitoa maelezo mbali mbali kuhusu kilimo cha kutumia teknolojia.


. Matunda ya nyanya yakionekana shambani

WAKULIMA mbali mbali wa Mazao ya mbogamboga, maua na matunda wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini wametakiwa kuunganisha nguvu ili waweze kukidhi viwango vya uzalishaji wa mazao ya mboga mboga, matunda na maua kwa ajili ya kusafirisha nje ya Nchi.

Wito huo ulitolewa na Mkulima wa Nyanya wa Skimu ya Umwagiliaji ya Ilaji iliyopo Wilaya ya Mbarali mkoani hapa, Daniel Wabare, alipokuwa akizungumzia Changamoto zinazowakabili wakulima wa mazao hayo katika Sherehe za wakulima zilizoandaliwa na Taasisi ya TAHA zilizofanyika katika kijiji cha Ilaji.

Wabare alisema ili wakulima waweze kutumia fursa ya Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kusafirisha mazao ya Mboga mboga, matunda na maua ni lazima wakulima wanaounda Mikoa ya Nyanda za juu kusini yenye fursa hiyo wakaungana.

Alisema ili usafirishe mzigo mkubwa kwa ndege ni lazima bidhaa ziwe za kutosha jambo ambalo mtu mmoja hataweza kulimudu isipokuwa kwa kuunganisha nguvu, hivyo akatoa wito kwa Wakulima wenzie kuunda umoja utakaowawezesha upatikanaji wa masoko na uzalishaji wenye tija.

Wabare alisema chini ya uangalizi wa Shirika la TAHA aliweza kujifunza teknolojia ya kilimo cha nyanya cha umwagiliaji kwa njia ya matone wakati wa maonesho ya Wakulima nanenane mwaka huu baada ya kutembelea banda lao na hatimaye kujaribu kilimo hicho kilichomletea mafanikio makubwa.

Alisema katika Shamba la Hekta moja ameweza kupanda Nyanya tangu mwezi wa nane ambazo ameanza kuvuna mwezi huu huku matarajio yake ikiwa ni kupata matenga 560 yenye thamani ya shilingi Milioni 8.4 ili hali alitumia mtaji wa shilingi Milioni 2.6 kwa msaada wa TAHA.

Kwa upande wake Bwana shamba wa TAHA kutoka Makao makuu, Isaac Ndamanhyilu, alisema shirika lake limekuwa likiwafundisha Wakulima teknolojia mbali mbali zinazowasaidia kulima chenye tija kwa kulinga kuinua uchumi na kuinua vipato vyao pamoja na upatikanaji wa masoko.

Alisema baada ya kuwafundisha wakulima hao hutenga siku moja ambayo huwakusanya wakulima kutoka skimu mbali mbali ili waweze kubadilishana uzoefu changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za kilimo cha mazao ya Horticulture ili ziweze kutatuliwa na wataalamu wa Kilimo.

Katika Sherehe za Jana zilizofanyika katika Skimu ya umwagiliajo ya Ilaji iliyopo wilayani Mbarali iliwakutanisha wakulima zaidi ya 300 kutoka Skimu za umwagiliaji za Wilaya za Mbarali na Mbeya ambazo ni Moto mbaya, Ihahi,Ipatagwa,Chimala, Igomelo, Uturo na Simambwe.

Naye Mgeni rasmi katika Sherehe hizo, Afisa Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Alfred Mzurikwao, ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kiff, alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za TAHA katika kuwaendeleza wakulima kilimo chenye tija.

Alisema TAHA inafanya kile kinachopaswa kufanya na Serikali pamoja na kutekeleza agizo la Rais Kikwete kwa Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini ya kuhakikisha inajikita katika kilimo cha Matunda, Mboga mboga na maua ili kutumia fursa ya Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kusafirishia mazao yao.

Mwisho.

Na Mbeya yetu