Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Monday, October 20, 2014

HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA LAZINDUA KAMPENI YA CHANJO

 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla akizindua kampeni ya Chanjo jijini Mbeya hivi karibuni





HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya linatarajia kuwapatia chanjo watu zaidi ya Laki mbili wakiwemo watoto kuanzia miezi 9 mpaka chini ya miaka 15, miezi 6 mpaka miezi 59, kuanzia miezi 12 hadi miezi 59 na kuanzia miaka 5 na kuendelea.

Hayo yalibainishwa na Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro, wakati wa uzinduzi wa Chanjo hiyo iliyofanyika katika kituo cha Afya Ruanda kilichopo Mwanjelwa jijini hapa ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla.

Dk. Lazaro alisema kampeni ya chanjo hizo ni ya kitaifa ambapo zoezi hilo litadumu kwa muda wa wiki moja na kuzitaja aina za Chanjo hizo kuwa ni pamoja na Surua Rubella itakayowalenga watoto wa miezi 9 hadi miezi 59 wapatao 171,862, chanjo nyingine ni matone ya vitamin A itakayowalenga watoto kuanzia miezi 6 hadi 59 wapatao 62,772.

Alizitaja aina zingine za Chanjo kuwa ni dawa ya minyoo ya Mabendazole kwa watoto wote wenye umri wa miezi 12 hadi miezi 59 wapatao 50580 na dawa ya Invermectin na Albendazole zinazokinga Usubi, Minyoo ya tumbo matende na mabusha kwa wenye umri kuanzia miaka 5 na kuendelea wapatao  345110.

Aliongeza kuwa ili zoezi hilo lifanikiwe Halmashauri imeandaa vituo vingi vitakavyoendesha kampeni ya Chanjo na kuligawa katika aina mbili ambazo alizitaja kuwa ni vituo vya kudumu na vituo vya muda ambavyo watalaamu watakuwa wakihama hama kufuata watu walipo.

Alisema vituo hivyo vitakuwa 79 vikiwa na jumla ya watumishi 553 ambavyo alivitaja kuwa ni pamoja na Kliniki za huduma za afya ya uzazi na Mtoto, shule zote za msingi na Sekondari,Stendi za mabasi, Stesheni za Treni na sehemu yoyote itakayoonekana kufikika kiurahisi na jamii na sehemu yenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya mkusanyiko wa watu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla, aliwakemea wananchi wengi wanapotoshwa na imani potofu kuhusiana na chanjo hizo kwamba zinapunguza na kusababisha matatizo kwenye upande wa uzazi.

Alisema chanjo ni muhimu kwa watoto kwa sababu itamsaidia baadaye kutopata magonjwa ambayo hayatibiki kirahisi jambo litakalowagharimu wazazi na kuishia kulaumiana baada ya matatizo kutokea dhidi ya watoto wao.

Alisema utafiti unaonesha idadi kubwa ya watu wanaopata magonjwa ukubwani, kupoteza uwezo wa kufikiri na kuwa wasahaulifu wanakuwa hawakupata chanjo wakiwa watoto.

Alisema baadhi ya magonjwa kama Matende, mabusha, usubi na minyoo ya tumbo yanadhibitiwa kupitia chanjo pekee na kwamba kuyatibu baada ya kutokea ni vigumu kutokana na mwili kukosa chanjo tangu mwanzo.

Mwisho.


No comments: