Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, November 18, 2014

WAKULIMA WA MAZAO YA HORTICULTURE WAHAMASISHWA KUUNGANA.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Alfred Mzurikwao, akizungumza na wakulima mbali mbali alipokuwa amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbarali katika sherehe za Wakulima zilizofanyika katika skimu ya umwagiliaji ya Ilaji iliyoko Mbarali mkoani Mbeya.


Afisa wa TAHA, Isac Ndemanhile, akizungumza na wakulima zaidi ya 300 waliohudhuria sherehe za wakulima katika skimu ya Ilaji.

 Maafisa wa TAHA wakitoa maelezo kwa mgeni rasmi katika moja ya mashamba ya wakulima yanayoendeshwa kwa kufuata teknolojia mbali mbali.

Mkulima wa Nyanya, Daniel Wabare akionesha matunda ya shamba lake baada ya kupata elimu kutoka kwa maafisa wa TAHA.


 Baadhi ya wakulima wakiangalia mazao ya nyanya katika shamba la mmoja wa wakulima waliofundishwa na TAHA.

Baadhi ya wakulima kutoka skimu mbali mbali wakiwasikiliza maafisa wa TAHA wakitoa maelezo mbali mbali kuhusu kilimo cha kutumia teknolojia.


. Matunda ya nyanya yakionekana shambani

WAKULIMA mbali mbali wa Mazao ya mbogamboga, maua na matunda wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini wametakiwa kuunganisha nguvu ili waweze kukidhi viwango vya uzalishaji wa mazao ya mboga mboga, matunda na maua kwa ajili ya kusafirisha nje ya Nchi.

Wito huo ulitolewa na Mkulima wa Nyanya wa Skimu ya Umwagiliaji ya Ilaji iliyopo Wilaya ya Mbarali mkoani hapa, Daniel Wabare, alipokuwa akizungumzia Changamoto zinazowakabili wakulima wa mazao hayo katika Sherehe za wakulima zilizoandaliwa na Taasisi ya TAHA zilizofanyika katika kijiji cha Ilaji.

Wabare alisema ili wakulima waweze kutumia fursa ya Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kusafirisha mazao ya Mboga mboga, matunda na maua ni lazima wakulima wanaounda Mikoa ya Nyanda za juu kusini yenye fursa hiyo wakaungana.

Alisema ili usafirishe mzigo mkubwa kwa ndege ni lazima bidhaa ziwe za kutosha jambo ambalo mtu mmoja hataweza kulimudu isipokuwa kwa kuunganisha nguvu, hivyo akatoa wito kwa Wakulima wenzie kuunda umoja utakaowawezesha upatikanaji wa masoko na uzalishaji wenye tija.

Wabare alisema chini ya uangalizi wa Shirika la TAHA aliweza kujifunza teknolojia ya kilimo cha nyanya cha umwagiliaji kwa njia ya matone wakati wa maonesho ya Wakulima nanenane mwaka huu baada ya kutembelea banda lao na hatimaye kujaribu kilimo hicho kilichomletea mafanikio makubwa.

Alisema katika Shamba la Hekta moja ameweza kupanda Nyanya tangu mwezi wa nane ambazo ameanza kuvuna mwezi huu huku matarajio yake ikiwa ni kupata matenga 560 yenye thamani ya shilingi Milioni 8.4 ili hali alitumia mtaji wa shilingi Milioni 2.6 kwa msaada wa TAHA.

Kwa upande wake Bwana shamba wa TAHA kutoka Makao makuu, Isaac Ndamanhyilu, alisema shirika lake limekuwa likiwafundisha Wakulima teknolojia mbali mbali zinazowasaidia kulima chenye tija kwa kulinga kuinua uchumi na kuinua vipato vyao pamoja na upatikanaji wa masoko.

Alisema baada ya kuwafundisha wakulima hao hutenga siku moja ambayo huwakusanya wakulima kutoka skimu mbali mbali ili waweze kubadilishana uzoefu changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za kilimo cha mazao ya Horticulture ili ziweze kutatuliwa na wataalamu wa Kilimo.

Katika Sherehe za Jana zilizofanyika katika Skimu ya umwagiliajo ya Ilaji iliyopo wilayani Mbarali iliwakutanisha wakulima zaidi ya 300 kutoka Skimu za umwagiliaji za Wilaya za Mbarali na Mbeya ambazo ni Moto mbaya, Ihahi,Ipatagwa,Chimala, Igomelo, Uturo na Simambwe.

Naye Mgeni rasmi katika Sherehe hizo, Afisa Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Alfred Mzurikwao, ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kiff, alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za TAHA katika kuwaendeleza wakulima kilimo chenye tija.

Alisema TAHA inafanya kile kinachopaswa kufanya na Serikali pamoja na kutekeleza agizo la Rais Kikwete kwa Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini ya kuhakikisha inajikita katika kilimo cha Matunda, Mboga mboga na maua ili kutumia fursa ya Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kusafirishia mazao yao.

Mwisho.

Na Mbeya yetu

No comments: