Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, May 20, 2015

WANANCHI WA UKANDA WA ZIWA NYASA KUNUFAIKA NA UPATIKANAJI WA TAARIFA MAALUM ZA HALI YA HEWA

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bi. Theo Ntara ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kyela (watatu kutoka kushoto), Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt. Hamza Kabelwa (wa nne kutoka kushoto) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha inayohusu uboreshaji wa huduma za hali ya hewa katika maeneo ya Ziwa Nyasa kwa sekta ya wakulima na wafugaji, wavuvi na wasafirishaji, tarehe 14 Mei 2015 katika hotel ya Kyela Resort-Mbeya.

Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani kupitia mpango wa utoaji wa huduma za hali ya hewa wa GFCS yaani “Global Framework for Climate Services” imezindua rasmi  huduma ya kutoa taarifa za hali ya hewa hususan tahadhari na utabiri mahususi kwa watumiaji wa ziwa nyasa. Taarifa hizo zitasamabazwa kupitia vyombo mali mbali vya habari ikiwemo redio za kijamii. Huduma hiyo ilizinduliwa rasmi tarehe 11 Mei 2015 huko Kyela mkoani Mbeya na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dkt. Thea Ntara aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Katika kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu TMA wameandaa warsha ya “UBORESHAJI NA UAINISHAJI WA MAHITAJI YA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA MAENEO YA ZIWA NYASA KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI, WAVUVI NA WASAFIRISHAJI’’ iliyofanyika katika hotel ya Kyela Resort jijini Mbeya. Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bi. Thea Ntara alisema ‘Hivi karibuni tumeshuhudia matukio ya mvua ya mawe, mafuriko na radi katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mbeya, hali hii imesababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi. 

Nimatumaini yangu kuwa taarifa zinazopatikana kutoka kwa wananchi na wataalam mbalimbali kupitia semina hii zitaiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kuboresha taarifa zake kwa umma na kuwawezesha watalaam kutoa ushauri stahiki unaozingatia taarifa za hali ya hewa’. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa hali ya hewa wanaotumia ziwa nyasa iliyowajumuisha wasafirishaji, wakulima, wavuvi, wafugaji, Ofisi ya Bandari, SUMATRA,usalama, Maafa, maliasili na vyombo vya habari.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt Agnes Kijazi katika hotuba yake iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Utabiri TMA Dkt. Hamza Kabelwa alisema ‘Katika kuhakikisha TMA inazidi kuziboresha huduma zake, wataalam wa TMA wameweza kutembelea maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kyela ili kupata uelewa zaidi wa majanga yanayoikumbuka wilaya hiyo na namna gani ya kuweza kufanyia kazi’. 

 ‘TMA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari imejikita katika kuhakikisha jamii inapata taarifa za hali ya hewa kwa wakati hususan kunapokuwa na vipindi vya matukio  ya hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa, ukame, upepo mkali, mawimbi makubwa n.k  kwa lengo la kuisaidia jamii kuchukua tahadhari mapema ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na matukio hayo  hivyo kuchangia katika kuokoa maisha ya watu na mali zao’ alisema Dkt. Kijazi.

IMETOLEWA NA MONICA MUTONI AFISA HABARI MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.

No comments: