Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, November 4, 2015

SHITAMBALA ATOA YA MOYONI KUHUSIANA NA UCHAGUZI MKUU ULIOPITA MBEYA MJINI


Kapten Sambwee Shitambala akiwa katika moja ya mikutano ya Kampeni wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.


Kwanza napenda kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sote kumaliza kampeni na uchaguzi kwa usalama na amani bila kuibuka kwa vurugu za aina yoyote. Na hiii ilikuwa kauli mbiu yangu amani na usalama ndo msingi wa maendeleo ya nchi na jimbo letu.
Pili natoa shukurani kwa chama cha MapinduzI kwa kuniteua kupeperusha bendera ya chama changu katika uchaguzi mkuu kugombea ubunge jimbo la Mbeya mjini ambao ulihitimishwa Oktoba 25.
Pia nawashukuru wanahabari kwa msaada wao katika kuujuza umma wa Mbeya mambo yaliyokuwa yakijiri kwenye kampeni zetu tulizokuwa tukizifanya kwenye kata zote 36, nilifanikiwa kufanya jumla ya mikutano 56 na zaidi ndani na nje na niliweza kukutana na wananchi wengi maeneo mbalimbali niliyofanya kampeni na kusikiliza kero zao.
Nachukua fursa hii pia kuwashukuru wagombea wenzangu wote wa ndani ya chama wapatao 15 kwa kushirikiana nami katika Kampeni hizo. Shukrani za pekee zimwendee Charles Mwakipesile aliyekuwa Meneja wangu.
Pamoja na mimi kuteuliwa na chama bado wagombea wenzangu katika chama walijitahidi kuniunga mkono na kunisapoti kwa hali na mali wapo walioacha shughuli zao na kuzunguka nami kwenye kampeni zote jitihada zao zimeonekana, nawashukuru sana.
Navishukuru kipekee vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa, ngumu na nzuri waliyoifanya na kulifanya jiji letu la Mbeya kuwa salama hadi leo. Nawashukuru sana.
Nilijitahidi kufanya kampeni za kistaarabu, kwa kutumia uwezo wangu wote pamoja na matukio mbalimbali ya kejeli yaliyokuwa yakitolewa na wapinzani wetu, nilichukulia kama ndio siasa kwani kila mmoja alikuwa anatafuta kiti cha Ubunge wa Jiji la Mbeya kwa namna yake lengo letu lilikuwa moja kusukuma maendeleo ya Jiji letu.
Mwenzangu wa chadema ameibuka na kura nyingi zaidi ya wengine tuliogombea naye na kutangazwa kuwa mbunge mteule wa jiji la Mbeya. Haya ni maamuzi ya wana Mbeya wengi zaidi ya wale waliotaka niwe mbunge wao. Nampongeza Sugu kwa ushindi huo na pia ninamtakia kila laheri katika muda wake wa uongozI. Pamoja na dosari zilizojitokeza kwenye uchaguzi huu lakini nimekubaliana na matokeo, tuweke mambo ya itikadi pembeni tusimame pamoja tuijenge Mbeya yetu.
Kwa bahati mbaya sana nimeshindwa katika uchaguzi huu nikiwa nimekusanya takribani kura 50,000  inawezekana wakati bado haujafika wa mimi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya, nimefarijika kwa wale walionipa kura na hata wale ambao hawakunichagua,  Nawashukuru wananchi wote.
Najua walionichagua walinielewa, walinikubali,walihitaji niwawakilishe. Nasema nitawawakilisha na sitowatupa. Yale niliyoyasema yatatimia juu yao kwa namna moja ama nyingine kadri Mungu atakavyojalia. Sitawaacha wala kuwaangusha. Nawaomba wasijione wameshindwa na wasikate tamaa. Nipo nao pamoja. Ahadi nilizotoa wakati wa kampeni nitazitekeleza kwa kadri ambavyo Mungu atanijaalia.
Nipo na wanajamii hapa hapa Mbeya, shughuli zangu na biashara zangu zipo hapa Mbeya nitaendelea kuwa na wana Mbeya kwa hali na mali tukiendelea kulijenga Jiji letu la Mbeya.
Naahidi nitaendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo la Mbeya kwa hali na mali nikifuatilia na kutekeleza ahadi zilizoahidiwa na Rais mteule Dkt.John Pombe Magufuli, pamoja na kwamba sikuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Mbeya.Kwa niaba ya walionipigia kura nitafanya kazi.
Ndugu wanahabari nilijiwekea vipaumbele wakati wa kampeni zangu pamoja na ahadi kwa wananchi wa jimbo la Mbeya katika baadhi ya maeneo niliahidi mambo mbalimbali kama vile ujenzi wa zahanati kata ya Iyunga, Igawilo, Ilemi na Nsoho. Shule kata ya Iziwa, na zinginezo, usafiri wa daladala pembezoni, maji na umeme. Pia kutafuta waalimu wazuri kwa ajili ya shule zetu. Bila kusahau pembejeo kwa wakati. Nitashirikiana na wananchi katika kutekeleza ahadi zangu.
Pia zipo ahadi nilizoahidiwa na Rais wangu mteule ambaye ni muadilifu na mchapakazi nitamkumbusha ikiwemo km 10 za barabara Jiji la Mbeya na mengineyo ambayo nimeahidi kuyatekeleza mwenyewe kwa wapiga kura wakati wa kampeni. 
Ndugu zangu wanahabari, naamini mlikuwa mkitafakari kukaa kwangu kimya baada ya kumalizika kwa uchaguzi huu wengi walitegemea ningeweza kupinga matokeo, kufanya hivyo kungesababisha kuchelewesha mahitaji ya wakazi wa jiji la Mbeya ambao wanahitaji huduma yangu na ahadi nilizotoa kwa wengi waliojitokeza kuniunga mkono, nawaahidi sitawaangusha.
Mwisho lakini si kwa umuhimu napenda kuwasisitiza wakazi wa Jiji la Mbeya kuendelea kushikamana kwa ajili ya kuliendeleza jiji letu, tuepuke vishawishi na kujiingiza katika mambo ya uvunjifu wa amani na utulivu.
Amani ya Mbeya ikitoweka hakuna biashara inayoweza kufanywa wala hakuna shughuli zozote za maendeleo ambazo zinaweza kufanywa,vijana wajikite kwenye ujasiriamali watafute riziki yao halali kwa kuwa Mbeya yenye amani na salama kwa Maendeleo yetu linawezekana.
Ahsanteni
Capt. Sambwee Shitambala (MNEC-CCM, Mbeya)


No comments: